Monday, November 21, 2016

HATIMAYE CLEMENT SANGA AWEKA WAZI UJIO WA GEORGE LWANDAMINA YANGA SC

HATIMAYE CLEMENT SANGA AWEKA WAZI UJIO WA GEORGE LWANDAMINA YANGA SC

Makamu mwenyekiti wa Yanga SC leo asubuhi akihojiwa na waandishi wa habari , amefafanua kwa kina ujio wa kocha mpya George Lwandamina toka Zambia kuja kuwanoa mabingwa watetezi hao nchini.

" ni kweli tumeingia mkataba na George Lwandamina aliyekuwa akiifundisha Zesco United nchini Zambia . Lwandamina ataanza kuifundisha timu yetu mzunguko wa pili wa ligi kuu"

Sanga mbali na kuweka wazi suala hilo ambalo lilikuwa ni gumzo kwa vyombo vya habari nchini, pia ametoa maelezo ya kina kwa mustakabali wa aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo Hans Van Pluijm.

" mwalimu wetu Hans Van Pluijm bado tutaendelea kuwa nae kama mkurugenzi wa benchi la ufundi . Ni mwalimu mzoefu na anaijua vyema Yanga SC hivyo ushauri wake na uzoefu utakuwa chachu ya mafanikio katika benchi letu la ufundi na klabu kiujumla."

Hans Van Pluijm ameridhia nafasi hiyo baada ya uongozi wa klabu hiyo kukaa nae chini na kumwomba aendelee kubaki klabuni kwa nafasi hiyo adhimu kwa maendeleo ya klabu hiyo kimbinu na kiufundi.

Sanga amefafanua zaidi kwamba ; mabadiliko hayo hayana maana kwamba kiwango cha kocha wa awali bwana Pluijm kilikuwa kibaya bali uongozi katika hatua ya kuiboresha klabu yake umeamua kuleta changamoto mpya ili kujiweka bora zaidi katika michuano mbalimbali inayoikabili timu hiyo .

George Lwandamina anategemewa kujiunga mapema na klabu hiyo baada ya wachezaji kurudi likizo kwa maandalizi ya ligi . Likizo waliyopewa inakwisha tarehe 25 na uongozi unatarajiwa kuweka kambi nje ya nchi kwa maandalizi yakinifu ya mzunguko wa pili wa ligi kuu unaoanza rasmi Desemba 17.

Wakati huo huo makamu mwenyekiti amezungumzia hatima ya kocha msaidizi wa klabu hiyo ndugu Juma Mwambusi . Bado wanamtambua kama kocha msaidizi wa klabu hiyo mpaka hapo itakapotangazwa tofauti.

" mara nyingi kocha mkuu ndio anaamua au kupendekeza msaidizibwake na sio klabu hivyo bado Mwambusi ni kocha wetu mpaka hapo itakapotangazwa tofauti . Klabu kwa sasa imejikita kwa hao wawili wakubwa wa juu"

Hans Van Pluijm sanjari na Juma Mwambusi wameifikisha timu hiyo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu ikiwa nyuma ya wahasimu wao wakubwa Simba SC kwa tofauti ya alama 2 . Simba SC wanaongoza ligi wakiwa na alama 35 na Yanga SC 33.

Uongozi wa Yanga SC unaandaa siku maalumu ya kuwatambulisha George  Lwandamina kamw kocha mkuu na Hans Van Pluijm kama mkurugenzi wa ufundi wa klabu kwa wanachama , wapenzi na wadau wa soka nchini.

No comments:

Post a Comment